Barabara muhimu kufungwa Nairobi wakati wa kongamano la tabia nchi

Marion Bosire
2 Min Read

Barabara muhimu za jiji la Nairobi zitafungwa kati ya Jumatatu na Jumatano wiki ijayo wakati wa kongamano la Afrika kuhusu tabia nchi.

Kongamano hilo litaandaliwa Septemba 4 hadi 6, 2023.

Barabara hizo ni ile ya Harambee Avenue kutoka mzunguko wa Parliament hadi makutano ya barabara ya Taifa, barabara ya Taifa kutoka makutano ya Harambee Avenue hadi makutano ya City Hall Way, makutano ya barabara ya City Hallway kutoka mzunguko wa Holy Family Basilica hadi makutano ya barabara ya Taifa na barabara ya Parliament kutoka mzunguko wa Harambee Avenue hadi mzunguko wa City Hallway.

Zitafungwa kuanzia Jumatatu Septemba 4 saa nane usiku hadi Jumatano Septemba 6 saa 12 jioni.

Rais Wiliam Ruto atafungua rasmi kongamano hilo la ulimwengu katika jumba la mikutano ya kimataifa la KICC ambalo linakutanisha watu wapatao elfu 30 kutoka sehemu mbali mbali ulimwenguni.

Msongamano wa magari unatarajiwa kwenye barabara kuu za kuingia na kutoka jijini Nairobi kwa sababu wengi wa wageni watakaohudhuria kongamano hilo wataishi kwenye hoteli zilizo kwenye barabara hizo.

Wengi wamekodisha mahali pa kulala kwenye barabara ya kuelekea Thika, ile ya Ngong, ya kuelekea Mombasa na ya kuelekea Limuru kati ya nyingine.

Megesho ya magari jijini Nairobi kama vile ya KenyaRe, Mahakama ya Upeo, Holy Family Basilica na Charter Hall yamefungwa kwa matumizi ya umma na yatatumiwa na wageni wa kongamano hilo kwa siku hizo tatu.

Wahudumu wa magari ya uchukuzi jijini Nairobi hata hivyo wamehakikishia umma kuhusu kuendelea kwa shughuli zao kama kawaida bila tatizo lolote.

Share This Article