Waziri Ogamba aonya dhidi ya udanganyifu katika mitihani

Marion Bosire
1 Min Read
Julius Ogamba, Waziri wa Elimu

Waziri wa elimu Julius Migos Ogamba ameonya walimu wakuu wa shule na wanafunzi dhidi ya udanganyifu katika mitihani ya kitaifa inayoendelea.

Akizungumza jana katika hafla moja ya kuchangisha pesa katika kanisa la Nyagesenda SDA lililoko katika kaunti ndogo ya Marani kaunti ya Kisii, Ogamba alisema wanafunzi wamejiandaa vyema na wanafaa kuaminia uwezo wao wa kuafikia matokeo mazuri.

Waziri huyo alionya kwamba watakaopatikana wakihusika katika udanganyifu watachukuliwa hatua kali kisheria.

Aliwataka pia wadau wa elimu kusalia macho na kuripoti visa vyovyote vya kutia doa uadilifu wa mitihani hiyo kwa maafisa husika.

Wakati huo huo Ogamba alipongeza kanisa kwa kuwa kielelezo katika uongozi na kukuza jamii iliyo na maadili mema yaliyojikita katika unyenyekevu na huduma kwa wengine.

Baraza la mitihani ya kitaifa nchini KNEC linaandaa mitihani ya kitaifa sampuli tatu wa kwanza ukiwa wa mfumo unaoondolewa wa 8.4.4 wa kidato cha nne KCSE.

Mingine ni mitihani ya utathmini wa uwezo wa wanafunzi chini ya mtaala mpya wa CBC, ambayo ni ule wa Gredi ya sita KPSEA na ule wa gredi ya tisa KJSEA.

Website |  + posts
Share This Article