Waziri Ndung’u: Serikali kubuni mazingira bora katika sekta ya ICT

Martin Mwanje
2 Min Read
Dkt. Margaret Ndung'u - Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali

Serikali imedhamiria kubuni mazingira wezeshi yanayokuza uwekezaji na kubuni fursa katika sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT) kwa ajili ya ukuaji wa sekta zote.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali Dkt.  Margaret Ndung’u amesema kupitia ushirikiano na sekta ya kibinafasi, serikali inakusudia kubuni mazingira bora na jumuishi ya ICT ambayo yatachochea mabadiliko ya kidijitali nchini.

Amesema serikali inatambua wajibu muhimu unaotekelezwa na sekta ya kibinafsi katika kukuza ubunifu na kuendeleza uchumi wa kidijitali nchini.

Waziri aliyasema hayo leo Jumatatu wakati wa mkutano wa mashauriano na watoaji huduma za teknolojia nchini (TESPOK) uliofanyika jijini Nairobi.

Ametoa wito kwa washirika wa sekta ya kibinafsi kuendelea kuwekeza katika uvumbuzi, mafunzo na miundombinu itakayowezesha kizazi kijacho cha viongozi barani Afrika.

“Kuhusika kwenu ni muhimu katika kuhakikisha uchumi wa dijitali wa Afrika ni jumuishi na thabiti,” alisema Waziri Ndung’u.

Kulingana naye, mabadiliko yanayoendelea katika sekta hiyo ikiwa ni pamoja na mapitio ya mipangokazi ya udhibiti yanakusudia kuiweka upya sekta ya ICT katika nafasi ya kukabiliana na masuala ibuka na kuiongoza nchi katika siku za baadaye zenye uunganishaji uliobreshwa wenye tija.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Katibu wa ICT na Uchumi wa Dijitali Mhandisi John Tanui na mwenzake wa Utangazaji na Mawasiliano Prof. Edward Kisiang’ani miongoni mwa maafisa wengine wa ngazi za juu serikalini.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa TESPOK James Turuthi alitoa wito wa usaidizi wa serikali katika kuangazia changamoto zinazowakumba watoaji huduma katika sekta hiyo.

Aliongeza kuwa sekta ya kibinafsi inatazamia kushirikiana na serikali katika ustawishaji wa Mswada wa Miundombinu Muhimu ili kukabiliana na tatizo la uharibifu miongoni mwa changamoto zingine.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mwasiliano David Mugonyi na Afisa Mkuu Mtendaji wa Mamlaka ya ICT Stanley Kamanguya ni miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *