Vikosi vya usalama vyatibua shambulizi la ugaidi Mandera

Tom Mathinji
1 Min Read
Shambulizi la kigaidi latibuliwa Mandera.

Vikosi maalum vya usalama humu nchini vimetibua shambulizi lililoshukiwa kutekelezwa na wanamgambo wa Al-Shabaab kwenye kaunti ya Mandera.

Baada ya kupokea habari za kijasusi, vikosi hivyo vilianzisha oparesheni dhidi ya wanamgambo wa Al Shabaab, waliokuwa wakipanga kutekeleza shambulizi katika barabara kuu ya Alungu-Elwak.

Vitengo vya usalama vya kukabiliana na ugaidi vilisema kupitia mtandao wa X kwamba wanamgambo walikabiliwa baada ya kufumaniwa wakiweka vilipuzi katika barabara kuu vilivyoyalenga magari ya uchukuzi wa umma.

Maafisa hao wanawasaka washukiwa wengine waliotorokea kwenye vichaka vilivyokuwa karibu wakati wa oparesheni hiyo. Bunduki mbili aina ya AK-47 pamoja na vifaa vingine vilitwaliwa, hatua iliyotibua uwezekano wa kuzuka kwa shambulizi kubwa dhidi ya halaiki ya raia.

Shirika hilo limesema oparesheni hiyo iliyofaulu inadhihirisha kujitolea na uangalizi wa asasi za usalama za humu nchini katika vita dhidi ya ugaidi.

Website |  + posts
Share This Article