Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali Dkt. Margaret Nyambura Ndung’u amehudhuria maadhimisho ya siku ya wakfu wa Umoja wa Mataifa, UN leo Alhamisi katika afisi za umoja huo jijini Nairobi.
Akihutubia wanadiplomasia na watu wengine mashuhuri wakliokuwepo, Dkt. Ndung’u alisisitiza umuhimu wa UN kukuza ushirikiano na kushughulikia changamoto katika jamii.
Dkt. Ndung’u alipongeza juhudi zinazoendelea za UN za kutoa usaidizi wa kibinadamu, utunzaji wa mazingira na maendeleo endelevu.
Alisisitiza kujitolea kwa Kenya kuendelea kushirikiana na umoja huo katika mpango wa ruwaza ya mwaka 2030 na mipango mingine ya ulimwengu hasa katika eneo la upembe wa Afrika na eneo la maziwa makuu.
Waziri huyo alizungumzia mada ya maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya UN ambayo ni “kuleta mkataba nyumbani” ambayo alisema inalenga kubadili maazimio ya ulimwengu kuwa vitendo vya kufaidi kizazi cha sasa na kizazi kijacho.
Aliainisha msimamo makini wa Kenya kuhusu masuala muhimu kama ukosefu wa usawa na mabadiliko ya tabia nchi akitaja uwekezaji wa taifa hili katika nishati safi ambayo ni asilimia 91 ya umeme wote nchini.
Dkt. Ndung’u alihimiza ulainishaji bora pamoja na ushirikiano ili kusaidia jamii ambazo ziko kwenye mazingira magumu.
Alimalizia kwa kuhimiza kujitolea katika sekta mbalimbali ili kuwianisha mapatano ya siku za usoni kuhakikisha kila Mkenya na kila mtu ulimwenguni ana fursa ya kustawi.
Siku ya Umoja wa Mataifa huadhimishwa tarehe 24 mwezi Oktoba kila mwaka, kukumbuka siku ambayo mkataba wa UN ulianza kutumika mwaka 1945.