Waziri Nakhumicha awapongeza wafanyakazi katika Wizara ya Afya

Tom Mathinji
2 Min Read
Waziri wa Afya Susan Nakhumicha.

Waziri wa Afya Susan Nakhumicha amewahimiza wafanyakazi wote katika wizara yake kuunga mkono mpango wa afya kwa wote kuambatana na ajenda ya mageuzi ya kiuchumi ya Bottom-Up.

Akiwahutubia wafanyakazi hao siku ya Jumatano katika Jumba la Afya Jijini Nairobi, Waziri Nakhumicha aliwahakikishia wafanyakazi hao kwamba amejitolea kuboresha maslahi yao ya kikazi.

“Ni mwaka mmoja sasa tangu nilipojiunga na wizara hii, na ninawapongeza nyote kwa jinsi mlivyoniunga mkono. Ninahitaji ushirikiano wenu tutakapokuwa tukizindua mpango wa afya kwa wote wakati wa sherehe za Mashujaa mwezi ujao,” alisema Nakhumicha.

Katika mkutano huo, Waziri alikuwa ameandamana na Katibu katika Idara ya Huduma za Matibabu Harry Kimutai, Kaimu Mkurugenzi wa Afya Dkt. Patrick Amoth na mbunge wa Endebess Robert Pukose, miongoni mwa wengine.

Kwa upande wake, Pukose alimpongeza Nakhumicha kwa juhudi zake za kuleta mabadiliko yatakayoimarisha utendakazi wa wahudumu wa afya na pia kuboresha sekta ya afya hapa nchini.

Wafanyakazi katika wizara ya afya wahudhuria mkutano ulioongozwa na waziri Susan Nakhumicha.

Pukose ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya afya katika bunge la kitaifa, aliwahakikishia Wakenya kuwa bunge litapitisha miswada minne kuhusu afya kuambatana na ahadi za serikali ya Kenya Kwanza ya kuwapa Wakenya huduma bora za afya.

“Bunge limejitolea kuunga mkono kazi nzuri ya waziri ya kuimarisha ubora wa viwango vya afya. Hazina ya Bima ya Afya ya NHIF hivi karibuni itaondolewa na kuwekwa hazina ya bima ya kijamii ya afya, kuhakikisha kila Mkenya anapata huduma bora za afya,” alisema Pukose.

Kwa sasa, serikali inatafuta fedha za kuwasajili Wakenya wote katika bima hiyo mpya ya afya ya NSHIF.

Share This Article