Waziri wa michezo Salim Mvurya amewarai Wakenya kujitokeza kwa wingi kuishabikia Harambee Stars katika mchuano wa robo fainali dhidi ya Madagascar kuwania kombe la CHAN katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani.
Aidha, Mvurya ameipongeza Harambee Stars kwa kusajili matokeo mazuri ikiwemo ushindi wa bao moja kwa bila dhidi ya Zambia siku ya Jumapili katika mchuano wa mwisho wa kundi A uliowawezesha kuongoza kundi hilo.
Mvyura pia amepongeza ushirikiano kati ya vyombo vya usalama, kamati andalizi ya CHAN, shirikisho la FKF na wafadhili kwa kuhakikisha mechi zinaendeshwa jinsi inavyostahili.
Pia Waziri amesifia mashabiki waliotii amri ya serikali na kutazama mechi ya Jumapili katika maeneo sita yaliyotengwa na kuwekwa runinga.
Zaidi ya mashabiki 26,000, walifurika uwanjani Kasarani kutazama mechi ya Kenya na Zambia huku wengine wanaokisiwa kuwa zaidi ya 50,000, wakijumuika kwenye maeneo mbalimbali kutazama mechi kupitia runinga.
Harambee Stars, ambao ni waandalizi wenza wa CHAN, hawajapoteza mechi kati ya nne walizocheza licha ya kushiriki kipute hicho kwa mara ya kwanza na watachuana na Madagascar katika kwota fainali Ijumaa.