Waziri wa Michezo Kipchumba Murkomen ametetea wanariadha wa humu nchini dhidi ya ukosoaji ambao wamepitia katika siku chache zilizopita kufuatia matokeo yao katika michezo ya Olimpiki ya Paris, Ufaransa.
Wakenya walionyesha kutoridhika kwao kupitia mitandao na matokeo waliyoyataja kuwa duni ya wanariadha kwenye Olimpiki hata katika fani ambazo Wakenya wamekuwa wakitawala.
Akizungumza wakati wa kikao cha kiamshakinywa katika ikulu ndogo ya Eldoret, Murkomen alisema wengi wa Wakenya wanajua tu kusema mitandaoni ila hawajui wanayopitia wanariadha kujiandaa na kushiriki mashindano ya kimataifa.
Murkomen alisifia wanariadha hao akisema lilikuwa suala la kuridhisha kusikia wimbo wa taifa ukichezwa katika jukwaa la kimataifa mara nne kitu ambacho alisema hakiwezi kununuliwa popote.
Hata hivyo, Murkomen alisema ni muda mwafaka kwa serikali na viongozi kuwapa wanariadha usaidizi wanaohitaji ili waafikie matokeo bora katika mashindano kama hayo siku za usoni.
Alilaumu kutowajibika kwa mashirika mbalimbali ya michezo nchini akisema kwamba Kenya ingekuwa inashiriki mashindano mbalimbali kuliko riadha pekee ili kujihakikishia medali zaidi.
Waziri huyo alitaja michezo kama vile uogeleaji, upigaji mishale na mingine ambayo ina mashirikisho simamizi nchini ambayo Kenya inaweza kushiriki kimataifa.