Waziri Murkomen asema ajali za barabarani zitapungua

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri wa uchukuzi na Barabara Kipchumba Murkomen.

Waziri wa uchukuzi Kipchumba Murkomen amesema amechukua jukumu kuhakikisha idadi ya ajali za barabarani zinapungua katika barabara za hapa nchini.

Waziri aliahidi kutekeleza agizo la Rais William Ruto la kukomesha visa vya ajali barabarani vilivyoongezeka na ambavyo vimesababisha vifo vya watu wengi na majeruhi.

Kwa msingi huu, waziri Murkomen aliwaonya madereva, waendeshaji bodaboda na abiria dhidi ya kukiuka sheria za trafiki, akidokeza kuwa maafisa wa polisi wamepewa maagizo ya kutekeleza sheria hizo kikamilifu bila kuzingatia idara wanazohudumia.

“Kufuatia agizo la Rais William Ruto, maafisa wote wa polisi wanapaswa kutekeleza agizo hilo bila kujali idara wanazotoka. Watakaokiuka sheria za trafiki watakuwa mashakani. Idadi ya ajali lazima ishuke,” alisema Murkome.

Wakati wa uzinduzi wa mpango wa kitaifa kuhusu usalama barabarani hapo jana, Rais William Ruto alisema kwamba serikali itaboresha miundo msingi, kukabiliana na kutojali na kuimarisha uhamasisho kuhusu usalama barabarani kama mbinu za kupunguza ajali za barabarani.

Kadhalika Rais, alisema kuwa serikali itawekeza katika teknologia ya kisasa ya kufuatilia trafiki ili kudumisha usalama katika barabara zote za humu nchini.

Share This Article