Waziri mkuu wa taifa la Ireland Leo Varadkar ametangaza kwamba amejiuzulu kama kiongozi wa chama tawala cha “Fine Gael”.
Katika tangazo hilo la kushtukiza la leo Jumatano, Varadkar alielezea kwamba ataachia pia wadhifa wa waziri mkuu punde baada ya mwingine kuteuliwa.
“Ninajiuzulu kutoka kwa wadhifa wa kiongozi wa chama cha Fine Gael na nitajiuzulu pia kama waziri mkuu punde baada ya mwingine kuteuliwa.” Varadkar aliambia wanahabari katika jiji kuu Dublin.
Mwaka 2017, Varadkar aliandikisha historia ya kuwa waziri mkuu wa kwanza ambaye ni shoga katika nchi hiyo ambayo ilikuwa inaongozwa pakubwa na mafundisho ya kanisa Katoliki.
Alikuwa pia mtu wa umri mdogo zaidi kuwahi kushikilia wadhifa wa waziri mkuu ambao alirejelea pia mwaka 2022.
Katika mkutano na wanahabari leo, Leo alisema kwamba alipokubali kuongoza chama na kuwa waziri mkuu mwaka 2017, alijua kwamba katika uongozi mtu anahitajika kufahamu muda wa kupitisha uongozi kwa mtu mwingine.
Kulingana naye muda huo ni sasa.