Waziri Mkuu wa Bangladesh ajiuzulu na kukimbilia India

Martin Mwanje
1 Min Read

Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina ameripotiwa kujiuzulu na kukimbilia nchini India. 

Hasina amejiuzulu wakati ambapo maelfu ya waandamanaji nchini humo wameingia barabarani katika mji mkuu Dhaka siku moja baada ya makabiliano makali kati ya polisi na waandamanaji kusababisha vifo vya watu wapatao 90.

Baadhi ya waandamanaji wameripotiwa kuvamia makazi ya Hasina mjini Dhaka.

Watu wapatao 300 wameripotiwa kuuawa katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita huku mamlaka ikikabiliana na waandamanaji wanaoipinga serikali.

Kufuatia kujiuzulu kwa Hasina, Mkuu wa jeshi la Bangladesh amehutubia taifa kupitia televisheni muda mfupi uliopita.

Waker-uz-Zaman amesema serikali ya mpito itaundwa.

Aliongeza kuwa atakutana na Rais Mohammed Shahabuddin, na kwamba ana matumaini kuwa “suluhisho” lingepatikana mwisho wa siku.

Mkuu huyo wa jeshi alisema tayari amezungumza na vyama vya upinzani vya kisiasa nchini humo.

Haijabainika nani ataongoza serikali.

Waker-uz-Zaman ameapa “haki” kwa watu wote wa Bangladesh – jambo ambalo waandamanaji wamekuwa wakidai kufuatia vifo vya mamia ya watu wiki chache zilizopita.

Share This Article