Waziri Linturi asema Kenya imejitolea kuhakikisha uwepo wa chakula

Marion Bosire
1 Min Read

Waziri wa kilimo na ufugaji Mithika Linturi amesema serikali ya Kenya imejitolea kuhakikisha uwepo wa chakula salama na bora kwa wote kwa kuwianisha mipango yake ya upatikanaji wa chakula na malengo endelevu.

Linturi ambaye anahudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa wa kukadiria mifumo ya chakula nchini Italia pamoja na Naibu Rrais Rigathi Gachagua, alisema Kenya imebuni mikakati ya kuwa na mifumo endelevu, sawa kwa wote, yenye afya na stahimilivu ya chakula.

Kulingana naye, haya yataafikiwa kupitia utekelezaji wa mpango mahsusi wa mabadiliko na ukuaji wa sekta ya kilimo wa mwaka 2019-2029.

Alisema ukosefu wa chakula unasababishwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi kama misimu inayobadilikabadilika ya mvua na ukame wa muda mrefu ambavyo husababisha mazao ya kilimo ya kiwango cha chini.

Waziri huyo alisema kwamba mipango ambayo serikali imebuni ili kuhakikisha uwepo wa chakula nchini ni pamoja na mpango wa mbolea ya bei nafuu na kuongeza uzalishaji. Mipango hiyo imepigwa jeki na msimu wa mvua na sasa Kenya inatarajia mavuno mengi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *