Madai kwamba maafisa wa Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS na maafisa wengine wa usalama wanahusika katika mauaji ya kiholela au kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya umma au mtu yeyote ni ya uongo na hayana msingi.
Waziri wa Usalama wa Taifa Prof. Kithure Kindiki anasema madai hayo yamedhamiria kupotosha umma kuhusiana na vurugu zilizoshuhudiwa katika baadhi ya sehemu za nchi wakati wa maandamano yaliyoshuhudiwa katika siku za hivi karibuni.
Muungano wa Azimio na mashirika kadhaa ya kutetea haki za binadamu yamewanyoshea maafisa wa usalama kidole cha lawama yakiwatuhumu kwa kutekeleza mauaji ya kiholela na kutumia nguvu kupita kiasi wakati wa maandamano yaliyoitishwa na upinzani na yaliyokumbwa na vurugu tele.
“Wanaoeneza uongo huu wanawajibika zaidi katika kupanga, kufadhili na kutekeleza uhalifu huu mkubwa uliosababisha vifo na majeraha kwa raia na maafisa wa usalama na uharibifu mkubwa wa mali ya umma na binafsi katika kipindi cha wiki chache zilizopita,” alisema Prof. Kindiki katika taarifa leo Jumanne.
“Taasisi za upelelezi na ujasusi zinatathmini ushahidi madhubuti walio nao, ushahidi ambao unatosha kuwafungulia mashtaka wapangaji wakuu, watekelezaji na wafadhili wa uchomaji wa makusudi wa kiwango kikubwa, wizi wa mabavu na uharibifu wa miundombinu, pamoja na vifo na kujeruhiwa kwa raia na maafisa wa usalama.”
Waziri Kindiki aliongeza kuwa imebainika silaha za raia zilizo na leseni na zisizokuwa na leseni zilizotolewa na watekelezaji wakuu wa vurugu zilizoshuhudiwa siku chache zilizopita zilitumiwa kuua na kuwajeruhi raia na maafisa wa usalama, na lawama kuelekezwa kwa maafisa wa usalama.
Amesema wapangaji wakuu wa vurugu hizo watawajibishwa siku, wiki na miezi ijayo.