Waziri Kindiki asema wahusika wa maandamano wataadhibiwa

Marion Bosire
2 Min Read

Waziri wa mambo ya ndani Kithure Kindiki ametoa taarifa kuhusu maandamano yaliyofanyika leo katika sehemu mbali mbali za nchi.

Kindiki kwenye taarifa hiyo ya Jumatano jioni, anasema wameunda kundi la maafisa wa vitengo mbali mbali vya usalama ambalo litafanya uchunguzi wa haraka. Watakaopatikana na hatia wakiwemo waliopanga maandamano,waliofadhili maandamano na waliosaidia kufanikisha kile anachokitaja kuwa uhalifu watakamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa mujibu wa sheria.

Kindiki analaumu Raila Odinga na wafuasi wake akisema kwenye maandamano ya leo kulishuhudiwa vurugu, uporaji na uharibifu wa mali na hata vifo vya waandanaji.

Kulingana na Kindiki Raila tangu jaribio la kupindua serikali mwaka 1982 na vurugu za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007, amekuwa akiongoza wafuasi wake kutenda vitendo ambavyo hutumbukiza nchi hii pabaya.

Aligusia pia yaliyoshuhudiwa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 ambayo anasema yalikuwa njama ya Raila ya kuingia kwenye serikali. Anasema ujio wake serikalini wakati huo ulisababisha matumizi mabaya ya fedha na hivyo nchi ikajilimbikizia madeni.

Raila Odinga alitangaza kufutiliwa mbali kwa mkutano wa hadhara ambao ulikuwa umepangiwa kufanyika katika uwanja wa Kamukunji leo. Alisema walipata taarifa za kijasusi kwamba upande wa serikali ulikuwa na mpango wa kupeleka wahuni kwenye mkutano wao wa amani ili kuuvuruga.

Kiongozi huyo wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya anahimiza wananchi kufanya maandamano kila Jumatano Ili kushinikiza serikali kupunguza gharama ya maisha kati ya matakwa mengine.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *