Waziri wa Usalama wa Taifa Kithure Kindiki amesema atafanya kila awezalo kuwafurusha wahalifu katika Bonde la Ufa.
Amesema hatakoma kuwasaka wahalifu waliojihami kwa silaha katika kaunti sita za Kaskazini mwa Bonde la Ufa au kuruhusu wahalifu waliofurushwa kujikusanya tena.
Aliyasema hayo wakati akikagua hatua iliyopigwa katika ujenzi wa barabara ya Tangul-Kolomogon kuelekea Keren.
Mnamo mwezi Machi mwaka huu, serikali ilitangaza kaunti sita za eneo hilo kuwa zinazokumbwa na ukosefu wa usalama na hatari na kutangaza operesheni ya kuwasaka wahalifu.
Kaunti hizo ni pamoja na Turkana, Pokot Magharibi, Elgeyo Marakwt, Baringo, Laikipia na Samburu.
“Yeyote atakayejaribu kuingia katika maeneo yaliyotengwa kwa kisingizo cha kutafuta malisho ya mifugo hataruhusiwa,” alionya Kindiki jana Jumatatu akiwa katika eneo la Kiserian, kaunti ya Baringo.
Aliongeza kuwa operesheni ya Maliza Uhalifu itaendelea kutekelezwa kwa muda mrefu na atafanya kila awezalo kuwazuia wahalifu kuingia katika maficho yao katika vilima vya Korkoron, Arabal, Bonde la Tandare na maeneo mengine ya mbali ambayo awali yalitumiwa kuwaficha wahalifu.