Waziri wa barabara na uchukuzi Davis Chirchir, amefafanua kwa Kamati ya bunge la seneti kuhusu barabara na uchukuzi kwamba hakuna makubaliano yaliyopo kati ya mamlaka ya viwanja vya ndege nchini – KAA na kampuni ya India ya Adani.
Ufafanuzi huo unafuatia hatua ya kampuni ya Adani ya kuwasilisha pendekezo lililoafikiwa kwa faragha tarehe 1 Machi 2024, ambalo bado linatathminiwa kwa lengo la kuafikia makubaliano yanayoweza kutekelezwa.
Chirchir alieleza kuwa Adani Airport Holdings Limited ya India iliwasilisha pendekezo la kujenga, kusimamia na kuhamisha uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta – JKIA chini ya mpango wa ushirikiano wa serikali na kampuni ya kibinafsi.
Kuhusu ardhi waziri huyo alisema Adani haitapatiwa ardhi ingawaje pendekezo la kampuni hiyo linahusisha ombi la ardhi ya kujenga mji karibu na JKIA.
Kulingana naye ombi hilo limeondolewa kwenye makubaliano na litazingatiwa kando kulingana na sera za KAA kuhusu ukodishaji na makubaliano.
Chirchir alielezea mipango ya kukarabati kituo kilichopo na kujenga kituo kipya cha abiria chenye uwezo wa kuhudumia watu milioni 23, na miundombinu ya kusaidia kama vile barabara za kuingia, maegesho, njia za kutoka haraka na ujenzi wa njia ya pili ya ndege kupaa.
Alisisitiza kuwa miundo na ramani za kina zitapatikana baada ya eneo la maendeleo kufafanuliwa, kusubiri kusainiwa kwa makubaliano hayo.