Wazazi wawaondoa wanafunzi katika shule ya wasichana ya Eregi

Tom Mathinji
1 Min Read

Wazazi wamewaondoa watoto wao katika shule ya wasichana ya Eregi iliyoko kaunti ya Kakamega, baada ya shule hiyo  kuathiriwa na ugonjwa usiofahamika siku ya Jumanne.

Ugonjwa huo ambao bado haujabainishwa, umesababisha wanafunzi 95 kulazwa katika hospitali mbali mbali katika kaunti ya Kakamega, huku wasimamizi wa shule hiyo wakitoa wito wa utulivu.

Wanafunzi walioathiriwa na ugonjwa huo walionyesha dalili za kuwa na maumivu kwa magoti na hivyo kushindwa kutembea.

Sampuli za damu, mkojo na kinyesi zimechukuliwa na kutumwa katika maabara ya Kisumu na katika taasisi ya utafiti wa kimatibabu-KEMRI jijini Nairobi kwa uchunguzi wa kina, huku majibu yakitarajiwa kutolewa leo Jumatano.

Kulingana na waziri wa afya kaunti ya Bernard Wesonga, wanafunzi  29  wanatibiwa katika hospitali ya Iguhu, 39  katika hospitali ya rufaa ya Kakamega, 31 katika hospitali ya misheni ya Mukumu na 14 katika hospitali ya Shibwe.

“Baadhi ya wanafunzi wameanza kupata nafuu huku wengine wakiendelea kupokea matibabu,”alisema Wesonga.

Mkurugenzi wa elimu katika eneo hilo Obiero Jared, alihakikishia umma kwamba hali hiyo imedhibitiwa.

TAGGED:
Share This Article