Watu wawili wamekamatwa kwa madai ya kujaribu kuwahonga maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI.
Katika taarifa, DCI inasema Jama Hirbo na Tasu Hirbo walijaribu kuwahonga maafisa hao kutoka kitengo cha kukabiliana na uhalifu wa kimataifa waliopo katika makao makuu ya idara hiyo kwa kitita cha shilingi 50,000.
“Wawili hao walikamatwa wakitekeleza kosa hilo papo hapo katika eneo la Huruma, kaunti ya Nairobi wakijaribu kuwahonga maafisa hao ili kutafuta kuachiliwa kwa washukiwa wa ulanguzi wa binadamu wanaozuiliwa katika kituo cha polisi cha Isinya katika kaunti ya Kajiado,” imesema DCI katika taarifa.
“Washukiwa walisafirishwa haraka hadi kituo cha polisi cha Muthaiga ili kuandikisha taarifa huku fedha walizopania kutoa kama hongo zikichukuliwa kwa lengo la kutumiwa kama ushahidi.”