Tume ya Uchaguzi nchini Uganda imetoa hakikisho kwa wagombea urais kuhusu muda wa uteuzi na ufaafu wao.
Haya yanajiri wakati uteuzi unatarajiwa kuanza leo Jumanne, Septemba 23, 2025. Tume hiyo ilieleza jana Jumatatu kuwa wagombea bado wana muda wa kutimiza masharti yanayohitajika.
Naibu Msemaji wa EC, Julius Mucunguzi, alithibitisha kuwa timu za EC zimekuwa zikifanya kazi ya kuhakiki orodha za wafuasi zilizowasilishwa na wagombea.
“Tume bado ina muda, timu zina muda. Tume imewajulisha wagombea wote waliokwisha kuchukua fomu za uteuzi na kurejesha orodha za wafuasi, kwamba hii ndiyo hali yao kwa sasa kuhusiana na kutimiza masharti,” alisema.
“Baadhi yao wameenda tena na tayari wanaendelea kukusanya sahihi zaidi. Kadri sahihi mpya zinavyowasili, timu huanza kuzihakiki mara moja na kisha kuwajulisha kiwango cha ulinganifu (compliance) ambacho wamefikia.”
Hadi sasa, wagombea wawili pekee ndio waliopitishwa: Yoweri Museveni wa NRM na Nathan Nandala Mafabi wa FDC. Zaidi ya wagombea 30 walikataliwa wiki iliyopita.
Mgombea wa NUP, Bobi Wine, alikuwa miongoni mwa waliokataliwa wiki iliyopita. NUP ilipokea taarifa kutoka EC kwamba uwasilishaji wao wa awali haukuwa na sahihi za kutosha. Habari hizo zilisababisha harakati za dharura za uhamasishaji. Mamia ya watu walikusanyika wikendi iliyopita katika ofisi za NUP jijini Kampala kutoa sahihi.
Katibu Mkuu wa chama hicho, David Lewis Rubongoya, alisema mwitikio wa wananchi ulikuwa juhudi ya kijamii.
Alisema watu kutoka wilaya mbalimbali, wakiwemo wasio wanachama wa NUP, walijitokeza kutoa msaada. Alithibitisha kuwa chama kimekusanya sahihi za kutosha, na walilenga kuwasilisha sahihi za ziada kwa EC.
Sheria inamtaka mgombea kuwa na angalau wafuasi 100 kutoka wilaya 98, ambazo ni theluthi mbili ya wilaya zote za Uganda.
Mucunguzi aliwaomba wagombea kuwa na imani na tume. Alisema EC ina jukumu la kufanya uhakiki wa kina ili kubaini iwapo wagombea wametimiza sifa zinazohitajika.