Wawakilishi wadi Nairobi waapa kumtimua Gavana Sakaja

Martin Mwanje
2 Min Read
Wawakilishi wadi wa Nairobi wakati wakiwahutubia wanahabari Septemba 1, 2025

Chuma cha Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja huenda ki motoni, siku chache baada ya mwenzake wa Kericho Erick Mutai kuponea chupuchupu shoka la kutimuliwa madarakani kwa mara ya pili. 

Hii ni baada ya wawakilishi wadi wa Nairobi (MCAs) kuapa kuwasilisha hoja ya kmtimua Sakaja madarakani kwa madai ya utepetevu kazini.

Wakiimba nyimbo za kudhirihisha azimio lao, wawakilishi hao wameelezea imani kwamba watakusanya saini zaidi ya 100 kama ishara kwamba imani yao kwa Gavana huyo imefifia.

“Tumeamua kumpiga teke Sakaja, na kamwe hatutarudi nyuma,” waliimba MCAs hao wakati moshi wa kumfurusha Gavana huyo madarakani ukizidi kuifunika anga ya Nairobi.

“Tunasema kwamba ili Nairobi iwork tena, Sakaja must go! Ili barabara zijengwe, Sakaja must go!”

Kinara wa hoja ya kumbandua Sakaja madarakani ni MCA wa Kileleshwa Robert Alai.

Wanamtuhumu Gavana huyo kwa kuwacha taka itawale kila pembe ya kaunti hiyo na kwa kushinda kuboresha miundombinu kwa manufaa ya wakazi, miongoni mwa tuhuma zingine.

Wawakilishi wadi hao wakiripotiwa kuwa makini kuhakikisha mchakato wao wa kumtema Sakaja unaendeshwa kwa uangalifu wa hali ya juu ili usije ukapigwa kumbo katika Bunge la Seneti kama ilivyotokea wakati wa mashtaka dhidi ya Gavana Mutai na mwenzake wa Isiolo Abdi Guyo.

Wanasema wameshapitisha idadi inayohitajika ya MCAs 42 kuhakikisha Sakaja anafunganya virago na kwenda zake.

Website |  + posts
Share This Article