Watu wawili walisombwa na maji ya mafuriko katika eneo la Sakutiek, kaunti ndogo ya Narok ya Kati, Jumanne usiku.
Akithibitisha kisa hicho, kamanda wa polisi kaunti ndogo ya Narok ya Kati John Momanyi, alisema wawili hao walikuwa wakijaribu kuvuka eneo ambalo lilikuwa na mafuriko, waliposombwa na maji ya mto wa msimu.
Miili ya wawili hao ilipatikana na wananchi waliokuwa wakishirikiana na maafisa wa polisi kuitafuta, na ilipelekewa katika chumba cha wafu katika hospitali ya kaunti ndogo ya Naivasha ikisubiri kufanyiwa upasuaji.
Kufuatia kisa hicho, afisa huyo mkuu wa polisi aliwaonya wakazi dhidi ya kuvuka maji ya mafuriko wakati huu wa msimu wa mvua.
Kwingineko ng’ombe wanane walifariki baada ya kupigwa na radi katika kijiji cha Mararianta, kaunti ndogo ya Narok Magharibi.
Ng’ombe hao walikuwa wakijikinga mvua chini ya mti, kisa hicho kilipotokea.