Wawakilishi wadi Meru waombwa kukatalia mbali mswada wa kuthibiti vileo

Marion Bosire
1 Min Read

Chama cha wafanyabiashara katika kaunti ya Meru, wamiliki wa hoteli na mabaa katika kaunti ya Meru wameomba wawakilishi wadi wa kaunti hiyo wasiidhinishe mswada wa kudhibiti vileo wa mwaka 2023 uliowasilishwa katika bunge la kaunti hiyo wiki jana.

Wakizungumza mjini Meru wakati wa kikao cha ushirikishi wa umma katika mswada huo, wanabiashara hao walisema asili ya mswada huo ni afisi ya naibu Rais na kwamba unalenga kuwaadhibu na kuwakandamiza.

Mkurugenzi wa bodi ya kudhibiti vileo katika kaunti ya Meru Mbaabu Muguna alisema kwamba mswada huo hauwezi kupitishwa Meru kwa sababu kaunti hiyo tayari ina sheria ya kudhibiti vileo ambayo anaitaja kuwa bora kuliko mswada huo uliopendekezwa.

Wamiliki wa hoteli na mabaa hawajafurahishwa na yaliyomo kwenye mswada uliopendekezwa wakisema unalenga kuwakandamiza na kuwaongezea ada fulani.

Wanasisitiza kwamba utoaji wa leseni za kuuza vileo umegatuliwa na hivyo kaunti za eneo la mlima Kenya ambazo bado hazijaunda sheria za kudhibiti sekta hiyo zipatiwe muda wa kufanya hivyo badala ya kulazimishwa kupitisha mswada huo.

Mswada huo unasemekana kuwasilishwa katika mabunge kadhaa ya kaunti za eneo la mlima Kenya na wawakilishi wadi wa maeneo hayo wanaripotiwa kuukataa.

Share This Article