Wawakilishi Wadi Kiambu wamtetea Gavana Wamatangi

Martin Mwanje & Antony Kioko
1 Min Read
Gavana Kimani Wamatangi

Baadhi ya Wawakilishi Wadi wa Bunge la Kaunti ya Kiambu wamemtetea vikali Gavana Kimani Wamatangi kufuatia tuhuma za ufisadi zinazomkabili.

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC inamchunguza Wamatangi kuhusiana na kashfa ya shilingi bilioni 1.27 zinazohusiana na zabuni anayodaiwa kupewa kupitia jamaa wake alipohudumu kama Seneta wa kaunti hiyo mnamo mwaka 2017.

Hata hivyo, wakizungumza katika eneo bunge la Githunguri jana Jumapili, Wawakilishi Wadi hao walidai tuhuma za EACC zimechochewa kisiasa na zinakusudia kuudhofisha utawala wa Gavana huyo.

Wakiongozwa na Naibu Spika ambaye pia ni Mwakilishi wa Wadi ya Hospital John Ndichu, Wawakilishi Wadi hao waliilaumu EACC kwa kutumiwa kama chombo cha kupigana vita vya kisiasa.

Waliahidi kumuunga mkono Wamatangi na kuwataka wapinzani wake kisiasa kujiepusha na kampeni za mapema kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 ili kumruhusu Gavana huyo kuwahudumia wakazi bila vikwazo.

Kwa upande wake, Wamatangi alisema shinikizo la kisiasa linalomkabili linatokana na msimamo wake wa kukatalia mbali ufisadi.

EACC imewasilisha faili kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, DPP ikipendekeza kushtakiwa kwa Magavana watatu wanaohudumu kwa sasa, akiwemo Gavana Wamatangi.

 

Martin Mwanje & Antony Kioko
+ posts
Share This Article