Wawakilishi wa kike wa kaunti zote 47 bungeni, wamesisitiza haja ya wanawake kushabikia vita dhidi ya ukeketaji, mimba za mapema pamoja na ndoa za mapema.
Walikuwa wakizungumza katika shule ya upili ya wasichana ya Suswa huko Narok Mashariki, kaunti ya Narok wakati wa kuzindua mpango wa Inua Jamii.
Viongozi hao wa kike walisema kuna haja ya kulinda watoto wa kike na kuhakikisha wanakamilisha masomo yao.
Kila mmoja wa wabunge hao waliohutubia wanafunzi na wanajamii wa eneo hilo alikuwa na himizo kwa jamii ya Maasai kwa lengo la kuhakikisha ukuaji wa mtoto wa kike.
Mwakilishi wa kaunti ya Kiambu bungeni Anne Wamuratha aliwataka wajane kulinda mali waliyoachiwa na waume zao wasikubali itwaliwe na watu wengine.
Rebecca Tonkei mwakilishi wa kaunti ya Narok alisema kwamba eneo la Narok Mashariki linaongoza kwa idadi ya wasichana wanaoacha shule katika kiwango cha asilimia 51.
Alihimiza wasichana wajitahidi kukamilisha masomo yao.