Wavinya: Nitawaangamiza wafisadi wote kaunti ya Machakos

Tom Mathinji
1 Min Read
Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti.

Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti amesema atakabiliana na walaghai na wafisadi katika kaunti ya Machakos anaosema wanawanyima haki wakazi wa kaunti hiyo.

Akizungumza aliporejea nchini jana Jumatatu baada ya ziara ya wiki tatu nchini Uingereza, Wavinya aliwaonya walaghai wote kuwa chuma chao ki motoni, na kwamba atahakikisha hawapati mwanya wa kupunja mali ya serikali ya kaunti hiyo.

“Ninafahamu kuwa wafisadi na walaghai hawafurahii kazi ninayofanya ya kuwafaidi wakazi wa Machakos. Nitakaza kamba na kuwatimua kutoka kwa mapato ya kaunri hii.”

Gavana huyo aliongeza kuwa, “Tunawafahamu, hatutakubalia kuwanyima watu wa Machakos haki yao ya kupata huduma.”

Wakati huo huo, Wavinya alipuuzilia mbali madai kwamba alizuiliwa nchini Uingereza kutokana na ulanguzi wa fedha.

“Nilikuwa nchini Uingereza pamoja na Magavana wengine ambako nilikuwa nikitafuta vifaa vya kuzima moto, kabla ya kuanza kushughulikia binti yangu aliyekuwa akijiunga na chuo kikuu. Sikuwa nimetiwa nguvuni.”

Aliwalaumu wapinzani wake wa kisiasa kwa kueneza habari za uwongo katika mitandao ya kijamii kwamba alikuwa ametiwa nguvuni kutokana na ulanguzi wa fedha.

Website |  + posts
Share This Article