Chama cha kitaifa cha wauguzi (KNUN), kimesitisha mgomo wa wanachama wake katika kaunti ya Migori, baada ya kutia saini makubaliano ya kurejea kazini.
Wauguzi hao walimaliza mgomo huo ulioanza Oktoba 28, 2024, baada ya kusema kuwa Gavana Nyaribo amekubali kutatua maswala yanayowaathiri.
Katibu Mkuu wa chama hicho Morris Opetu, alisema wauguzi kaunti ya Nyamira, walilalamikia uhaba wa wauguzi, hatua iliyosababisha wauguzi waliopo kufanya kazi kupita kiasi, pamoja na utepetevu wa serikali ya kaunti hiyo kutekeleza mkataba wa makubaliano wa awali.
Katika mkataba wa kurejea kazini, serikali ya kaunti hiyo ilikubali kuwapandisha vyeo wauguzi 83, na kukamilisha mchakato huo kufikia Machi 31, 2025.
Wakati huo huo, Gavana Nyaribo aliwahakikishia wauguzi walioajiriwa hivi karibuni watapokea malimbikizi yao, punde tu bajeti ya ziada ya mwaka 2024/25 itakapoidhinishwa.
Kwa upande wake katibu huyo mkuu wa KNUN aliitaka serikali kuwasikiliza wahudumu wa afya na kutatua mahitaji yao, bila ya kusubiri kutokea kwa migomo.