Mkuu wa utumishi wa umma Felix Koskei,amewaonya watumishi wa umma dhidi ya kujihusisha na ufisadi, la sivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Akiongea wakati wa mkutano wa wasimamizi wa vitengo vya ununuzi katika taasisi za umma hapa Nairobi, Koskei alisema ufisadi umekuwa kizingiti kikuu dhidi ya ustawi wa taifa hili.
Wakati wa mkutano huo uliojumuisha wakuu 60 wa mashirika tofauti ya umma, mkuu huyo wa utumishi wa umma aliwaonya vikali dhidi ya kushiriki uovu huo.
Koskei aliongeza kuwa utawala wa Kenya Kwanza umejitolea kuwaadhibu vikali maafisa wa umma wanaoshiriki ufisadi,bila kujali nyadhifa zao serikalini.
Alitoa wito kwa taasisi zote kushirikiana na serikali katika kukabili kero hilo la ufisadi.
Taasisi za umma zilitakiwa kuzingatia matumizi ya teknolojia na kudumisha uwajibikaji ili kutekeleza malengo yao.