Watu wawili wasombwa na maji ya mafuriko Narok

Wananchi waliokuwa wakishirikiana na polisi waliopoa miili ya wawili hao ambayo imehufadhiwa katika hospitali ya kaunti ndogo ya Naivasha.

Marion Bosire and Stanley Mbugua
1 Min Read

Watu wawili walisombwa na maji ya mafuriko katika eneo la Sakutiek, Kaunti Ndogo ya Narok Central usiku wa kuamkia leo.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti hiyo ndogo John Momanyi, alisema wawili hao walikuwa wakijaribu kuvuka eneo lililokuwa limefurika waliposombwa na maji kuelekea eneo la chini la mkondo wa maji hayo.

Miili ya marehemu hao ilipatikana na wananchi waliokuwa wakishirikiana na polisi katika zoezi la kuiopoa na kusafirishwa hadi hospitali ya kaunti ndogo ya Naivasha kwa ajili ya kuhifadhiwa ikisubiri upasuaji wa maiti.

Kufuatia tukio hilo, mkuu huyo wa polisi aliwataka wakazi kujiepusha na kuvuka mito iliyojaa maji msimu huu wa mvua ili kuepuka hatari.

Katika tukio jingine, ng’ombe wanane walifariki baada ya kupigwa na radi katika kijiji cha Mararianta, kaunti ndogo ya Narok Magharibi.

Ng’ombe hao waliokuwa mali ya Peter Sasiet walikuwa wakijikinga chini ya mti kufuatia mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha katika eneo hilo wakati mkasa ulitokea.

Matukio haya yanajiri wakati idara ya utabiri wa hali ya hewa imetabiri kwamba mvua kubwa itaendelea kunyesha katika maeneo mengi ya kaunti hiyo wiki hii.

Mito mingi katika kaunti ya Narok imefurika kufuatia mvua kubwa iliyonyesha kwa wiki mbili zilizopita na hivyo wakazi wanahimizwa kuwa waangalifu wanapojaribu kuvuka mito hiyo.

Website |  + posts
Stanley Mbugua
Share This Article