Watu 2 wajeruhiwa kwenye ufyatulianaji risasi kanisa la Lakewood, Marekani

Marion Bosire
2 Min Read

Watu wawili wameachwa na majeraha kufuatia kisa cha ufyatulianaji wa risasi katika kanisa la Lakewood jijini Houston nchini Marekani.

Wawili hao ni mtoto wa umri wa miaka karibu mitano na mwanamume wa umri wa miaka 57.

Mwanamke ambaye alikuwa amevaa koti refu, amejihami na bunduki ndefu huku akiwa na mtoto wa umri wa miaka mitano aliingia kwenye kanisa hilo linaloongozwa na mhubiri Joel Osteen Jumapili, Februari 11, 2024 na kuanza kufyatua risasi.

Maafisa wawili wa usalama ambao hawakuwa kwenye zamu, mmoja wa kituo cha polisi cha Houston na mwingine ambaye anahudumu kama wakala wa tume ya kudhibiti vileo katika jimbo la Texas, walimkabili mwanamke huyo wa umri wa miaka 30-35 kwa kufyatuliana naye risasi na kumuua.

Mkuu wa maafisa wa polisi katika eneo la Houston Troy Finner alisema kwenye mkutano na wanahabari kwamba kwa bahati mbaya, mtoto ambaye alikuwa ameandamana na mwanamke huyo aliumia vibaya kwenye makabiliano hayo.

Kisa hicho kilijiri dakika chache tu kabla ya saa nane alasiri kilingana na saa za nchi hiyo na haijulikani ni nani alifyatua risasi iliyoumiza mtoto.

Uhusiano wa mtoto na mwanamke huyo pia haujafahamika.

Mwanamume wa umri wa miaka 57 ambaye anaaminika kutohusika kwenye shambulizi hilo kwa vyovyote alipata jeraha la risasi kwenye mguu na alipelekwa hospitalini kwa matibabu, kulingana na Finner.

Walioshuhudia kisa hicho wanasema mwanamke huyo alitishia kwamba alikuwa amebeba bomu lakini baada ya kukabiliwa, polisi walitafuta kwenye gari lake na kwenye mwili wake na hawakupata kilipuzi cha aina yoyote.

Mhubiri Osteen alielezea kwamba shambulizi hilo lilitokea wakati walikuwa wamemaliza awamu moja ya ibada na walikuwa wanatarajia kuanza awamu nyingine na hilo lilisaidia kupunguza maafa.

Gavana wa jimbo la Texas Greg Abbott naye alitoa taarifa akisema wanasimama na walioathiriwa na kisa hicho kwa namna yoyote. Alisisitiza kwamba mahali pa ibada ni patakatifu.

Share This Article