Watu wawili wafariki katika ajali ya ndege ya mizigo China

Marion Bosire
1 Min Read

Watu wawili wamefariki katika ajali ya ndege ya mizigo iliyotokea mapema Jumatatu nchini China hususan jijini Hong Kong.

Ndege hiyo inaripotiwa kuteleza kutoka kwenye njia yake katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Hong Kong na kutumbukia baharini na kusababisha vifo hivyo.

Ilikuwa safarini kutoka Dubai wakati iliteleza na kugongana na gari la kushika doria uwanjani humo na waliofariki walikuwa ndani ya gari hilo, huku wahudumu wanne wa ndege hiyo wakinusurika.

Maafisa husika wameanzisha uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hiyo huku maswali yakiibuka kuhusu njia aliyochagua kufuata rubani punde baada ya kutua.

Wahudumu wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Hong Kong wanasema walitoa maelekezo stahiki kwa rubani na kuna ishara za maelekezo katika uwanja huo.

Steven Yiu mkurugenzi wa shughuli katika uwanja huo alielezea kwamba gari husika lilikuwa limeegeshwa nje ya njia ya ndege na kulikuwa na ua kati ya gari hilo na njia hiyo.

Anasema ndege hiyo ilipinda ikatoka kwenye njia yake ikaelekea kwenye ua huo, ikauharibu ikagonga gari hilo na kulisukuma hadi baharini.

Website |  + posts
Share This Article