Watu wanne washtakiwa kuhusiana na shambulizi Moscow

Marion Bosire
1 Min Read

Wanaume wanne wameshtakiwa mahakamani kuhusiana na shambulizi kwenye ukumbi wa burudani jijini Moscow nchini Urusi.

Walishtakiwa kwa makosa ya ugaidi kuhusu uovu huo uliotekelezwa dhidi ya watu waliokuwa wakihudhuria tamasha jijini humo.

Shambulizi hilo ambapo zaidi ya watu 130 walifariki limetajwa kuwa baya zaidi nchini Urusi kwa muda wa miongo miwili.

Watu wengine 182 waliachwa na majeraha na madaktari waliripoti kwamba yamkini 40 kati yao walikuwa katika hali mahututi.

Mahakama ya eneo la Basmanny jijini Moscow ilitambua wanne hao kama Dalerdzhon Mirzoyev wa umri wa miaka 32, Saidakrami Rachabalizoda wa miaka 30, Shamsidin Fariduni wa miaka 25 na Mukhammadsobir Faizov wa umri wa miaka 19.

Raia hao wa Tajikistan, walishtakiwa kwa shambulizi la kigaidi lililosababisha vifo, kosa ambalo adhabu yake ni kifungo cha maisha gerezani.

Wawili kati yao walikiri makosa hayo na wote wamezuiliwa rumande hadi Mei 22, 2024.

Share This Article