Watu kadhaa wajeruhiwa Tanzania kwenye makabiliano na polisi

Martin Mwanje & BBC
1 Min Read

Watu kadhaa wamejeruhiwa kwenye maandamano katika baadhi ya miji ya Tanzania huku shughuli ya upigaji kura ikiendelea katika uchaguzi mkuu ambao umekumbwa na mvutano.

Waandamanaji waliwasha moto barabarani, kuharibu mabasi, na kusababisha uharibifu mkubwa kwenye vituo vya mabasi ya mwendo kasi na miundombinu mingine ya umma.

“Tumechoka… Tunataka Tume huru ya Uchaguzi ili Watanzania wamchague kiongozi wanayemtaka,” mmoja wa waandamanaji aliiambia BBC.

Wapiga kura zaidi ya milioni 37 walisajiliwa kupiga kura katika uchaguzi wa urais na ubunge.

Vyama 16 vidogo, ambavyo havina umaarufu, vimeruhusiwa kugombea urais dhidi ya Rais Samia Suluhu, ambaye anawania muhula wa pili.

Mgombea pekee wa upinzani, Luhaga Mpina wa Chama cha ACT-Wazalendo, alienguliwa kutokana na taratibu za kisheria.

Awali, Rais Suluhu alipiga kura mapema leo asubuhi katika eneo la Chamwino na kuwataka raia kudumisha amani wakati wakipiga kura.

“Tuendelee kujitokeza, kama ambavyo mamilioni ya wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu wamefanya, na kupiga kura kwa amani na utulivu,” alisema Rais Suluhu anayetuhumiwa kwa kukandamiza vyama vikuu vya upinzani nchini humo.

 

Rais Samia Suluhu wa Tanzania akipiga kura Oktoba 29.
Martin Mwanje & BBC
+ posts
Share This Article