Maafisa wa Palestina wanasema kwamba jeshi la Israel liliua watu 64 wakiwemo watoto katika Ukanda wa Gaza wakati wa maadhimisho ya siku kuu ya Eid al-Fitr.
Shirika la Red Cresent la Palestina lilipata miili ya wahudumu wanane wa afya, wafanyakazi watano wa ulinzi na mfanyakazi mmoja wa shirika la umoja wa mataifa UN.
Haya yanajiri wiki moja baada ya magari ya wahudumu hao kushambuliwa karibu na Rafah kusini mwa Gaza.
Mashirika ya kimataifa ya Red Cross na Red Crescent yamelaani mauaji hayo yakisema yanawakilisha shambulizi baya zaidi dhidi ya wafanyakazi wake kote ulimwenguni tangu mwaka 2017.
Wizara ya afya ya Gaza imetoa takwimu za mashambulizi ya Israel katika ukanda wa Gaza tangu yalipoanza kufikia sasa ambapo watu 50,277 wameuawa na wengine 114,095 kujeruhiwa.
Hata hivyo, afisi ya vyombo vya habari ya Gaza ilisema yapata miezi miwili iliyopita kwamba idadi sahihi ya vifo hivyo ni 61,700, kutokana na idadi kubwa ya watu ambao hawajulikani waliko na wanaaminika kufa chini ya vifusi.
Katika shambulizi la Hamas la Oktoba 7, 2023 nchini Israel ambalo lilisababisha vita vya Israel huko Gaza, watu 1,139 waliuawa na wengine zaidi ya 200 wakashikwa mateka.
Huku hayo yakijiri, makundi ya kutetea haki nchini Hungary yamelaumu serikali ya nchi hiyo kwa mipango ya kumkaribisha waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu huku kukiwa na kibali cha kumkamata cha mahakama ya ICC.
Netanyahu anapangiwa kuzuru Hungary Jumatano huku wanaharakati hao wakitaka serikali imkamate kwani nchi hiyo ni mwanachama wa sheria za Roma zilizoasisi mahakama ya ICC.
Waziri huyo mkuu wa Israel na waziri wake wa zamani wa ulinzi Yoav Gallant wanasakwa na mahakama ya ICC kwa uhalifu dhidi ya binadamu huko Gaza.