Takriban watu 9 wamefariki na wengine watatu kujeruhiwa vibaya baada ya matatu walimokuwa wakisafiria kuhusika kwenye ajali ya barabarani, katika eneo la Kisumu ndogo katika barabara ya Londiani – Kisumu.
Katika ajali hiyo iliyotokea Jumanne alasiri, ilihusisha matatu ya kuwabeba abiria 14 iliyokuwa ikielekea Kisumu na lori lililokuwa likielekea upande wa pili.
Ripoti ya polisi, ilisema kuwa waliofariki walijumuisha wanawake wanne na wanaume watano.
Kulingana na taarifa ya polisi, ajali hiyo ilitokea baada ya dereva wa lori kupoteza mwelekeo katika eneo la Kisumu ndogo, na kugongana ana kwa ana na matatu hiyo.
Manusura wa ajali hiyo waliojumuisha mtoto na watu wawili wazima, walipelekwa katika hospitali ya kaunti ndogo ya Muhoroni kwa matibabu.
Dereva wa lori hilo alitoroka baada ya ajali hiyo, huku maafisa wa polisi wakimsaka.
Magari hayo mawili yalokokotwa hadi katika kituo cha polisi cha Kipsitet.