Watu 8 wauawa kufuatia mzozo wa ardhi Tana River

Tom Mathinji
2 Min Read

Watu wanane wameuawa katika kaunto ndogo ya Bangala, kaunti ya Tana River kufuatia mzozo wa ardhi.

Mauaji hayo ambayo yamesababisha hofu kubwa miongoni mwa wakazi wa eneo hilo, yalitokea katika maeneo ya Charidende, Nanigi na Anole.

Watu saba wanasemekana kuuawa jana Ijumaa na mmoja aliuawa leo Jumamosi.

Machafuko hayo pia yamesababisha kuchomwa kwa nyumba 20 katika maeneo ya Bula Vango na ardhi ya KBC.

Wakazi wa maeneo hayo sasa wanalaumu asasi za serikali za usalama kwa kutofika kwa wakati kutuliza hali.

Wakiongozwa na Mohamed Chora Said, aliyempoteza kaka yake katika machafuko hayo, wakazi hao wanatoa wito kwa Ispekta Jenerali wa polisi kuwahamisha maafisa wote wa polisi katika kituo cha polisi cha Madogo.

“Nilikuwa na ndugu yangu tuliposhambuliwa na watu waliokuwa na bunduki. Ndugu yangu alipigwa risasi wa kwanza mkononi, lakini singeweza kumuokoa kwa sababu nilikimbilia usalama wangu,huku wakiendelea kumpiga risasi mara kadhaa,” alisema Said.

“Kwanini maafisa wa usalama hapa wanawakubalia watu kuwa na bunduki na kuwaua watu wetu mchana peupe?. Hatuna imani na afisa anayesimamia kituo cha polisi hapa na tunataka ahamishwe,” aliongeza mkazi mwingine Swaleh Chereru.

Eneo hilo limeshuhudia changamoto za ardhi hasaa baada ya serikali kuwahamisha wakazi kutoka eneo la Mororo ambalo hukumbwa na mafuriko mara kwa mara na kuwapeleka karibu na barabara ya Junction- Bura.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article