Watu 45 wafariki kufuatia ajali ya basi Afrika Kusini

Dismas Otuke
1 Min Read

Watu 45 wamefariki nchini Afrika Kusini baada ya basi walilokuwa wakisafiria kuanguka takriban mita 50 kutoka kwenye daraja katika jimbo la kaskazini mwa nchi hiyo la Limpopo.  

Kulingana na vyanzo vya taarifa hiyo, ni msichana wa umri wa miaka minane pekee aliyenusurika, ingawa alipata majeraha mabaya na anapokea matibabu hospitalini.

Basi hilo lilianguka jana Alhamisi jioni kutoka darajani na kushika moto baada ya kugonga mwamba.

Abiria hao walikuwa mahujaji waliokuwa wakisafiri kutoka mji mkuu wa Botswana, Gaborone kuhudhuria ibada ya Pasaka mjini Moria.

Yamkini dereva wa basi hilo alishindwa kulidhibiti na kulisababisha kuanguka yapata kilomita 300 kaskazini mwa mji wa Johannesburg.

Serikali ya Afrika Kusini imejitolea kusaidia kusafirisha miili ya walioaga dunia hadi nchini Botswana.

Website |  + posts
Share This Article