Watu 38 wakufa maji baada ya mashua kuzama Yemen

Tom Mathinji
1 Min Read
Mashua yazama Yemen.

Takriban watu 38 kutoka eneo la upembe wa Afrika, wamefariki baada ya mashua yao kuzama katika pwani ya Yemen, maafisa wa eneo hilo wamesema.

Walionusurika wamewaambia waokoaji kuwa mashua hiyo iliyokuwa imebeba takriban watu 250 ilizama kutokana na upepo mkali.

Msako unaendelea kuwatafuta karibu watu 100 ambao bado hawajapatikana.

Mamlaka za mitaa huko Rudum, mashariki mwa Aden, zilisema kwamba waliokuwemo walikuwa wahamiaji, wengi wao kutoka Ethiopia, ambao hutumia Yemen kama njia ya kupita kuelekea maeneo ya Ghuba.

Hadi Al-Khurma, mkurugenzi wa wilaya ya Rudum, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa boti hiyo ilizama kabla ya kufika ufukweni.

“Wavuvi na wakaazi walifanikiwa kuwaokoa wahamiaji 78, ambao waliripoti kuwa wengine 100 waliokuwa nao kwenye boti moja hawapo.

“Msako bado unaendelea, na Umoja wa Mataifa umearifiwa kuhusu tukio hilo,” alisema.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, wahamiaji 97,000 waliwasili Yemen kutoka upembe wa Afrika mwaka jana.

Ongezeko hilo limetokea licha ya vita nchini Yemen na mashambulizi ya hivi karibuni ya Wahouthi dhidi ya meli zinazopitia bahari Nyekundu.

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *