Watu wapatao 22 wameripotiwa kufariki kufuatia shambulizi la angani katika mji wa Omdurman, nchini Sudan.
Shambulizi hilo linasemekana kuwa baya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini Sudan, tangu mapigano yalipozuka kati ya wanajeshi wa Sudan na kundi la RSF Aprili 15, 2023.
Taarifa ya wizara ya afya ya Sudan inaelezea kwamba shambulizi lilitekelezwa katika eneo la makazi la mji huo wa Omdurman ulio karibu na mji mkuu Khartoum.
Umoja wa Mataifa umelaani shambulizi hilo ambalo lilisababisha watu wengine wengi kupata majeraha.
Shambulizi sawia mwezi jana jijini Khartoum, lilisababisha vifo vya watu 17 wakiwemo watoto watano.
Lakini kundi la RSF, linasema kwamba vifo mjini Omdurman vilikua 31 na kulaumu jeshi kwa kutekeleza shambulizi katika eneo la makazi mjini humo.
Taarifa ya kundi hilo la RSF inalaani shambulizi hilo na kusema lilitekelezwa na waasi wakiongozwa na mkuu wa majeshi Abdel Fattah] al-Burhan.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani shambulizi la Jumamosi huku akizitaka pande husika kusitisha mapigano.
Wakazi wa Omdurman waliohojiwa walisema ni vigumu kufahamu upande uliotekeleza Shambulizi hilo. Walisema ndege za jeshi zimekuwa zikishambulia wanachama wa kundi la RSF katika eneo hilo na RSF pia wamekuwa wakitumia ndege zisizoendeshwa na rubani kujibu mashambulizi.