Watu wapatao 16 wamethibitishwa kufariki kwenye kisa cha moto katika jumba la biashara katika eneo la kusini magharibi mwa nchi ya China, haya ni kulingana na vyombo vya habari nchini humo.
Moto huo katika jumba la orofa 14 katika jiji la Zigong, mkoa wa Sichuan province, unaripotiwa kuzuka Jumatano usiku na wahudumu wa zima moto walisalia huko wakijaribu kuudhibiti hadi Alhamisi asubuhi.
Watu 75 waliokolewa kutoka kwenye jumba hilo.
Uchunguzi wa mwanzo unaonyesha kwamba shughuli za ujenzi ndizo zilisababisha moto huo lakini uchunguzi unaendelea ili kufahamu kisababishi halisi cha moto huo.
Video za mkasa huo zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha moshi mkubwa ukitoa kwenye dirisha za orofa za chini za jengo hilo kabla ya kusambaa na kufunika jengo zima.
Wazima moto walilazimika kutumia kila mbinu kuzima moto huo ikiwemo mbinu ya kunyunyizia jengo hilo maji kutoka angani kwa kutumia ndege.
Mikasa ya moto imesalia kuwa donda sugu nchini China ambapo kati ya mwezi Januari na Mei mwaka huu wa 2024, vifo 947 viliripotiwa nchini humo kutokana na visa mbali mbali vya moto.
Msemaji wa kitengo cha kitaifa cha kukabiliana na visa vya moto nchini China Li Wanfeng, anaelezea kwamba visa vya moto katika maeneo ya umma vimeongezeka hadi asilimia 40.
Vingi kati ya visa hivyo kwenye hoteli na mikahawa husababishwa na umeme, gesi ya kupikia na utepetevu.