Kenya imekumbwa na visa vitano vya vifo kutokana na ugonjwa wa homa ya Dengue, wengine takriban 2,000 wakiambukizwa.
Wizara ya Afya tayari imetoa tahadhari kwa wakazi wa kaunti za Garissa na Wajir baada ya jumla ya visa 1,678, vya watu walioambukizwa homa hiyo kuripotiwa.
Kulingana na Katibu katika Wizara ya Afya Mary Muthoni, kufikia Agosti 26 visa 95 vilikuwa vimeripotiwa katika kaunti ya Wajir kupitia kwa vipimo vya maabara.
Vifo vyote vitano viliripotiwa katika kaunti ya Garissa,vikiwemo vitano katika eneo la Garissa mjini na kimoja eneo la Hagadera.
Visa vingi katika kaunti ya Garissa vimeripotiwa Dadaab vikiwa jumla ya maambukizi 1,276, wakati Garissa mjini ikiwa na watu 251 walioambukizwa nayo Fafi ina 56.
Katika kaunti ya Wajir,Wajir Mashariki ina asilimia 85 na jumla ya aslimia 89.5 ya visa vyote vilivyoripotiwa nchini.
Watoto kati ya umri wa miezi sita na vijana wanaobaleghe wanajumuisha asilimia 46 ya visa vilivyoripotiwa katika kaunti ya Wajir na jumla ya asilimia 48.4 ya visa vyote kwa jumla.
Muthoni ameongeza kuwa serikali inachunguza kwa karibu maambukizi ya ugonjwa huo, ikiwataka watu kuondoa maji yaliyokwama karibu na makazi ,kufunika mitungi ya maji na kuwalinda watoto dhidi ya kuumwa na mbu wanaosababisha homa ya Dengue.
Homa ya Dengue husababishwa na Mbu aina ya Aedes, ambao hutembea sana mchana na kuwauma watu.