Maafisa 9 wa Wizara ya Fedha washtakiwa kwa ubadhirifu wa bilioni 1.5

Wote hao walikana mashtaka na kesi dhidi yao itatajwa tena Septemba 2 mwaka huu.

Martin Mwanje
2 Min Read
Maafisa wa Wizara ya Fedha walipofikishwa mahakamani Agosti 19 kwa madai ya ubadhirifu wa fedha

Mkugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma Renson Ingonga leo Jumatano amewashtaki mahakamani maafisa waandamizi wa Wizara ya Fedha na waasisi na wakurugenzi wa kampuni mbalimbali kwa madai ya ufujaji fedha wa hadi shilingi bilioni 1.5. 

Fedha hizo zilikuwa za Mpango wa Upelekaji wa Uvumbuzi na Teknolojia Mashinani (PROFIT) unaotekelezwa na Wizara ya Fedha kwa ufadhili kutoka kwa Mfuko wa Kimataifa wa Ustawi wa Kilimo (IFAD).

Washukiwa walikamatwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC jana Jumanne.

Nao walifikishwa mbele ya Hakimu Rose Ndobi wa Mahakama ya Kupambana na Ufisadi jijini Nairobi kwa madai ya ubadhirifu wa fedha za umma na wanakabiliwa na mashtaka 121.

Waliofikishwa mahakamani ni Nemwel Moturi Motanya (Mkuu wa Kitengo cha Uhasibu, Wizara ya Fedha), John Ngure Kabutha (Mratibu wa Mpango wa PROFIT), John Maina Muriithi (Mhasibu Mwandamizi, Wizara ya Fedha), Gladys Juliet Oroni (Mwasisi wa kampuni za Mawindo Enterprise, Brigs Agencies na Green Basils Agencies) na Brian Kiprop Chepkarat (Mwasisi wa Kampuni ya El Konyinta Technologies).

Wengine ni Ian Kwemoi Chepkarat (Mkurugenzi wa kampuni za 020 Investments Ltd na Vidi Vici Ltd), James Omwodo Ndai (Mwasisi wa kampuni za Ednas Agencies, Prozzep Technologies na Steeren Entreprises), Jimmy Carter Odoyo Osodo (Mwasisi wa kampuni ya Cadnic Investments) na Josphat Kamau Kamoshe (Mkurugenzi wa kampuni ya Blue Dart Agencies Ltd).

Wote hao walikana mashtaka na kesi dhidi yao itatajwa tena Septemba 2 mwaka huu.

Awali, EACC iliwataka washukiwa wengine kufika katika makao makuu ya EACC jijini Nairobi kuhusiana na sakata hiyo.

Washukiwa hao ni Billy Otieno Obango, Auma Ritah Otieno, Paul Mukasiali Shilaho, Susan Wangari Gathiaka na Erick Otieno Achila.

Miriam Roseline Obinda, Brown Mujenyi Agade, hilda Ndinda Ngava, Charles Cheruiyot na Jackline Kagai Saisi pia walitakiwa kufika EACC kuwajibikia vitendo vyao.

 

Share This Article