Huku maandalizi ya Kongamano la Mabadiliko ya Tabia Nchi Barani Afrika yakishika kasi, kundi linalohusika na masuala ya afya limeahidi kuhakikisha afya na usalama wa kila mmoja atakayehudhuria.
Kongamano la Tabia Nchi Barani Afrika mwaka 2023 litaandaliwa Septemba 4 hadi 8 jijini Nairobi.
Litahudhuriwa na watu mbalimbali kutoka kote ulimwenguni.
Kundi linaloshughulikia masuala ya afya linaangazia tahadhari za kiafya, kushughulikia dharura na ukaguzi wa maeneo kuhakikisha ulinzi wa afya ya umma linapoandaa mazingira mazuri kwa wote watakaohudhuria.
Ili kurahisisha mambo, Wizara ya Afya imesema itatoa magari ya ambulensi yenye vifaa vya kusaidia wenye dharura za moyo hasa kwa watu mashuhuri watakaokuwepo.
Magari ya ambulensi ya kawaida ya kuokoa maisha pia yatakuwepo kwenye maeneo yote ya kongamano hilo ili kutoa usaidizi iwapo kutatokea dharura.
Kliniki za muda pia zitakuwepo ili kushughulikia mahitaji mbalimbali ya washiriki ikiwa ni pamoja na wale wenye mahitaji maalumu.
Maafisa wa afya ya umma watakagua vilivyo maeneo ambapo wageni wataishi ili kuhakikisha yanatimiza viwango vinavyohitajika kiafya.
Kujitolea kwa Wizara ya Afya kuhakikisha usalama na afya wakati wa kongamano hilo ni dhihirisho kwamba imejitolea kuhakikisha mazingira salama kwa kila mmoja atakayehudhuria.
Dhamira ni kuhakikisha hafla hiyo inafanikishwa bila uwoga wa aina yoyote.