Watahiniwa milioni 2 kufanya mitihani ya kitaifa mwaka huu

Tom Mathinji
2 Min Read
Waziri wa elimu Julius Ogamba.

Wizara ya elimu imezindua rasmi kipindi cha mitihani ya kitaifa mwaka huu, ikisema kuwa jumla ya watahiniwa 2,279,414  watafanya mitihani hiyo.

Kulingana na wizara hiyo watahiniwa 1,303,913 watafanya tathmini ya shule za msingi KPSEA katika vituo 35,573, nao watahiniwa 965,501 wakifanya mtihani wa kidato cha nne KCSE katika vituo 10,565.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Jijini Nairobi, waziri wa elimu Julius Ogamba alisema wizara yake haitawahurumia wale ambao watajihusisha na wizi wa mitihani, akidokeza kuwa uovu huo huathiri ubora wa viwango vya elimu hapa nchini.

“Serikali haitakuwa na huruma kwa yeyote atakayepatikana akijihusisha na wizi wa mitihani,” alisema waziri Ogamba.

Kwa upande wake, katibu katika wizara ya elimu Dkt. Belio Kipsang, alitoa wito kwa wadau wote kuzingatia miongozo iliyotolewa na wizara hiyo kuepusha wizi wa mitihani.

“Tunatoa wito kwa washikadau wote kuzingatia kikamlifu kiongozo iliyowekwa kuhakikish hakuna wizi wa mitihani,” alisema Kipsang.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza la Kitaifa la Mitihani humu nchini (KNEC), Dkt David Njengere, alitoa hakikisho la usimamizi bora wa mitihani hiyo akisema KNEC imenunua makasha 41 mapya kwa ajili ya kuhifadhi na kusafirisha vifaa vya mitihani.

Wizara ya Elimu pia imevumbua ubunifu mpya katika juhudi za kudhibiti wizi na udanganyifu wa mitihani, miongoni mwao ikiwa ni kuchapisha jina la mtahiniwa kwenye karatasi ya maswali ya mtihani wa Kcse na kubadilishwa kwa zamu ya wasimamizi kila baada ya wiki mbili.

Mitihani hiyo itang’oa nanga tarehe 18 mwezi Oktoba hadi tarehe 22 mwezi Novemba mwaka huu.

Share This Article