Wataalam wapelekwa Hilliside Academy kuchunguza chanzo cha moto

Tom Mathinji
1 Min Read
Wataalam wa uchunguzi wapelekwa Hillside Academy, Nyeri.

Naibu Rais Rigathi Gachagua amesema kikosi cha maafisa wa upelelezi  kimebuniwa na kupelekwa katika shule ya Hillside Endarasha kaunti ya Nyeri, kuchunguza chanzo cha moto uliosababisha vifo vya wanafunzi 18.

Akizungumza alipozuru shule hiyo Ijumaa alasiri kufariji familia zilizowapoteza watoto wao, Gachagua alisema uchunguzi wa kina utafanywa huku ripoti ya uchunguzi huo ikitolewa kwa umma.

“Tumebuni kikosi maalum kutoka idara ya upelelezi wa makosa ya jinai DCI, wapasuaji wa maiti, wataalum wa kuchunguza mauaji na wataalm wa maabara na wako hapa. Tunaomba utulivu tuwapatie muda wafanye uchunguzi huo,” alisema Naibu huyo wa Rais.

Alitoa wito wa ushirikiano, ikizingatiwa kuwa sampuli zitachukuliwa kutoka kwa miili ili iweze kutambuliwa.

“Kutakuwa na shughuli nyingi za kufanyia miili uchunguzi wa DNA. Tunatoa wito wa ushirikiano kwa kila mmoja,” alisema Gachagua.

Gachagua wakati huo huo alitoa wito kwa wazazi ambao tayari wamewachukua watoto wao, kuripoti kwa maafisa wa serikali au shuleni humu, ili wajulikane walipo.

Share This Article