Maafisa wanne wanaohusishwa na usimamizi mbaya katika muungano wa vyama vya akiba na mikopo (KUSCO), watasalia korokoroni wakisubiri uamuzi iwapo wataachiliwa huru kwa dhamana mnamo Jumanne Februari 18,2025.
Washukiwa hao walitiwa nguvuni na maafisa wa upelelezi wa makosa ya jinai DCI, kama sehemu ya uchunguzi unaoendelea kuhusu usimamizi mbaya wa fedha uliosababisha kupotea kwa mabilioni ya fedha katika chama cha KUSCO.
Wanne hao George Magutu Mwangi, Mercy Muthoni Njeru, George Ochola Owino na Jackline Pauline Atieno Omolo, tayari walifikishwa katika mahakama za milimani Jijini Nairobi.
Wanakabiliwa na mashtaka ya wizi, ubadhirifu na utengenezaji wa stakabadhi bandia.
Wakati huo huo, Mahakama pia imemwita George Otieno Ototo ambaye ni Mkurugenzi wa zamani wa KUSCO, akitakiwa kusimama kizimbani siku ambayo kesi ya kuachiliwa huru kwa dhamana kwa washtakiwa wenzake wanne itakapokuwa ikisikizwa.