Wasimamizi wa viwanda na maghala ya kahawa wahimizwa kutumia polisi kwa ulinzi

Marion Bosire
2 Min Read

Wasimamizi wa viwanda vya kahawa na maghala nchini wamehimizwa kutafuta huduma za ulinzi wa viwanda hivyo kutoka kwa polisi waliojihami.

Haya yanafuatia matukio ya kila mara ya wizi wa zao hilo tukio la hivi karibuni zaidi likitokea katika ghala la chama cha ushirika cha wakulima wa kahawa cha Kaguru huko Meru ambapo kahawa ya thamani ya shilingi milioni 2.5 iliibwa.

Akizungumza alipozuru tawi la Meru la chama cha wakulima KPCU, mwenyekiti wa bodi ya chama hicho Daniel Chemno, aliwasihi wakulima wa Kahawa watafute huduma za polisi waliojihami kulingana na maelekezo ya wizara ya mambo ya ndani ili kulinda mazao yao.

Chemno alitenga chama cha KPCU na matamshi ya Zablon Mbabu mwenyekiti wa chama cha wanaosaga kahawa Meru aliyesema kwamba wizi wa zao la kahawa nchini unasababishwa na chama cha KPCU.

Mwenyekiti huyo wa KPCU alisema kwamba mwanzo wa mwaka, waziri wa mambo ya ndani aliwataka wahusika wa maghala ya zao la kahawa na mashamba ya zao hilo kutafuta huduma za polisi kulinda maeneo hayo.

Huku akiwataka polisi kuchunguza wizi uliotokea huko Kaguru, Chemno alisema KPCU haikuhusika kwa vyovyote na akamtaka Mbabu aombe msamaha hadharani au achukuliwe hatua za kisheria.

Mbabu amefafanua kwamba hahusishi wakulima wote na wizi huo bali ni watu fulani pekee na amesema hataomba msamaha na yuko tayari kwa hatua yoyote itakayochukuliwa dhidi yake.

Mkurugenzi mtendaji wa KPCU Timothy Mirugi alisema wameshuhudia ongezeko la maombi ya ufadhili kutoka kwa hazina ya mazao na kufikia sasa wamesambaza jumla ya shilingi Bilioni 1.9.

Kulingana naye, mfumo tofauti wa ugawaji wa pesa za hazina hiyo utazinduliwa karibuni ili kuongeza pesa ambazo mkulima anaweza kupata kutoka shilingi 20 kwa kila kilo hadi shilingi 40 kwa kila kilo.

Mirugi alielezea pia ongezeko la kiwango cha kahawa ambayo KPCU inasaga kwa kuwa inasaidia vya vingine vya ushirika ishara kwamba mabadiliko katika sekta hiyo yanazaa matunda.

Alisema wanunuzi wa moja kwa moja sasa wanaingia nchini sula ambalo linaonyesha kwamba kahawa haitakuwa ikisalia kwenye maghala kwa muda mrefu.

Share This Article