Wasimamizi wa shule waagizwa kuhakikisha usalama wa wanafunzi

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu.

Waziri wa elimu Ezekiel Machogu, amewaagiza wakuu wa shule kuhakikisha usalama wa wanafunzi ambao tayari wamewasili shuleni.

Serikali siku ya Ijumaa, iliaahirishwa kufunguliwa kwa shule kwa muda usiojulikana, kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvu kubwa inayoshuhudiwa nchini Kenya.

Aidha waziri huyo alidokeza kuwa shule zinafaa tu kuwaruhusu wanafunzi hao kurejea nyumbani iwapo hali haitawaruhusu kuendelea kukaa shuleni.

Machogu alitoa mwongozo huo muda mfupi baada ya Rais William Ruto kuagiza kuahirishwa kwa tarehe ya kufunguliwa shule kwa muda usiojulikana kutokana na mvua inayoendelea kunyesha inayosababisha mafuriko.

Na ili kuhakikisha mazingira shwari ya masomo wakati shule zitakapofunguliwa, waziri aliwaagiza maafisa wa elimu wanaofanyakazi katika shule ambazo zinawahifadhi watu walioathiriwa na mafuriko, kushirikiana na maafisa wa serikali ya taifa kuwatafutia watu hao makazi mbadala.

Baadhi ya wanafunzi waliripoti shuleni siku ya Jumatatu kufuatia utata baada ya waziri wa elimu kutoa ilani ya kuahirishwa kwa tarehe ya kufungua shule mnamo dakika za mwisho mwisho.

Hadi kufikia sasa shule 1,967 zimeharibiwa na mafuriko ambayo yamesababisha maafa ya watu 210 huku maelfu ya watu wakiachwa bila makao na sasa wamehifadhiwa katika baadhi ya taasisi za elimu.

Share This Article