Rais wa Tanzania Daktari Samia Suluhu Hassan amewataka wasimamizi wa michezo nchini humo kuwa makini ili kuhakikisha weledi katika uendeshaji wa shughuli za michezo.
Alikuwa akizungumza katika ikulu ndogo ya Tunguu huko Zanzibar aliposhiriki chakula cha mchana na timu ya Zanzbar ya soka ya wavulana walio chini ya umri wa miaka 15 inayojulikana kama Karume Boys.
Karume Boys ndio mabingwa wa kanda wa mashindano ya CECAFA kwa wachezaji walio chini ya umri wa miaka 15 na kikao hicho kilikuwa cha kuwapongeza.
Rais Samia alitaja michezo kuwa biashara kubwa na kushauri viongozi wabadilike na waache kuvuna wasikopanda.
Aliwataka kuhakikisha mipango endelevu ya kuwekeza katika vijana wanamichezo, mabaraza ya michezo yaendelee kuratibu na kufuatilia utendakazi wa Vyama vya michezo na kuhakikisha vinaendeshwa na kujiendesha kwa manufaa ya Taifa.
Kiongozi huyo wa nchi ya Tanzania alisema pia kwamba viwanja vya michezo vinafaa kutumika kwa uangalifu na ukarabati ufanywe mara tu matatizo madogo yanapotokea humo badala ya kusubiri matatizo hayo yakithiri.
Alisimulia kuhusu kisa ambapo aliwasilishiwa mahitaji ya fedha za kukarabati uwanja wa taifa akashangaa ni kwa nini shirikisho la soka halingesimamia gharama hiyo ilhali huwa linalipisha wote wanaoingia kutizama mechi.
Rais Samia hakutoa fedha za kugharamia ukarabati huo bali alielekeza shirikisho hilo litafute fedha na kutekeleza ukarabati uliokuwa unahitajika.
Lakini kwa sasa serikali kuu nchini humo inakarabati viwanja vyote kwa sababu ya mashindano yajayo ya AFCON mwaka 2027.
Hata hivyo Rais Samia anashikilia kwamba jukumu la ukarabati wa viwanja ni la wanaotumia viwanja hivyo.