Wasichana 5,000 kunufaika na visodo na elimu ya maisha

Marion Bosire
1 Min Read

Wasichana 5,000 watanufaika na ufadhili wa  visodo, mafunzo kuhusu kubalehe na ujuzi wa maisha kwa jumla, kufuatia ushirikiano kati ya afisi ya Mke wa Rais kupitia mpango wake wa “Mama Doing Good” na kampuni ya Proctor & Gamble.

Afisi ya Mke wa Rais kupitia kwa Dkt. John Chumo, Mkurugenzi Mkuu wa mpango wa Mama Doing Good, ilipokea shehena ya kwanza ya visodo katika Ikulu ya Nairobi, kutoka kwa Joyce Kariuki, Meneja wa Mahusiano na mipango mingine katika eneo la Afrika Mashariki kwenye kampuni ya Proctor & Gamble.

Ushirikiano huu na afisi ya mkewe rais ni sehemu ya mpango wa Proctor & Gamble wa kuhakikisha watoto wa kike wanasalia shuleni almaarufu “Always Keep Girls In School Initiative”.

Mpango huo hushirikisha mashirika mengine katika kufikia watoto wa kike wa gredi ya  sita hadi nane ambapo wanawapa visodo, mafunzo kuhusu kubalehe na ujuzi wa maisha kupitia kwa wauguzi.

Tangu kuanzishwa kwake, mpango huo umefikia wasichana milioni 10 nchini Kenya na ushirikiano huu utanufaisha wasichana katika maeneo yaliyotengwa na familia zilizo katika mazingira magumu kufurahia masomo, kuboresha kiwango cha wasichana wanaojiunga na shule za sekondari na kuwawezesha kujithamini maishani.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *