Maafisa wa Upelelezi wa Makosa ya jinai (DCI) leo Alhamisi wamewakamata washukiwa watatu kuhusiana na shambulizi dhidi ya Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi.
Seneta huyo alishambuliwa alipokuwa katika mkahawa mmoja Jijini Kisumu siku ya Jumatano.
Washukiwa hao waliokamatwa Carlos Owiti almaarufu Kalonje mwenye umri wa miaka 24 kutoka eneo laNyalenda, Eric Otieno almaarufu Dude (39) kutoka Manyatta, na Vincent Odhiambo almaarufu Tinga (27) kutoka Nyalenda, kwa sasa wamezuiliwa katika korokoro za polisi, wakisubiri kufikishwa mahakamani.
Kupitia ukurasa wa X, DCI ilisema imeimarisha uchunguzi, huku maafisa wakiendelea kuwatafuta washukiwa wengine wanaohusishwa kwa shambulizi hilo.
DCI iliwashukuru wananchi kwa kutoa habari zinazofanikisha uchunguzi unaoendelea, ikiwahimiza kuendelea kushirikiana zaidi ili kuhakikisha wahusika wote wa shambulizi hilo wanatiwa mbaroni.
Mapema Alhamisi wakazi wa kaunti ya Vihiga waliandamana barabarani kulalamikia shambulizi dhidi ya Seneta huyo, wakitaka waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria.